Full Description
Ahkaam-ul-Janaaiz
Mlango:
Bid´ah Za Jeneza
Kabla ya kufa
1- Baadhi ya watu wanaitakidi kwamba Mashaytwaan wanamjia yule ambaye anataka kukata roho kwa sura za wazazi wake wawili, mfano wa mayahudi na manaswara ili wamletee wao kila aina ya mila isiyokuwa ya Uislamu ili wampoteze. Anasema Ibn Hajar al-Haythamiy katika ”Fataawaa al-Hadiythiyyah” akinukuu kutoka kwa as-Suyuutwiy:
”Hilo halikupokelewa.”
2- Kuweka msahafu kwenye kichwa cha yule anayetaka kukata roho.
3- Kumlakinia[1] maiti akariri tamko la Mtume na maimamu wa Ahl-ul-Bayt (´alayhimus-Salaam).
4- Kumsomea Suurat Yaasiyn yule anayetaka kakata roho.
5- Kumuelekeza yule mwenye kukata roho Qiblah.
Hili amelikataza Sa´iyd Ibn Musayyib.
Baada ya kufa
6- Kauli ya Shiy´ah wanasema:
“Mwanaadamu anakuwa najisi wakati anapokuwa maiti isipokuwa wale ambao wamekingwa na madhambi,[2] shahidi na yule ambaye imemuwajibikia kuuawa akawa ameoga kabla ya kuuawa. Akauawa kwa sababu hiyo.”
7- Kumtoa mwanamke mwenye hedhi, damu ya nifasi (uzazi) na mwenye janaba kutoka kwa yule maiti.
8- Kuacha kufanya kazi kwa yule ambaye amehudhuria wakati ambapo roho ya maiti ilipokuwa inatoka mpaka zimpitikie siku saba.
9- Wanaitakidi baadhi ya watu ya kwamba roho ya maiti inaogelea pembezoni mwa mahali ambapo alikufa maiti.
10- Kuacha mshumaa (taa) liwake kwa maiti usiku alipofariki mpaka asubuhi.
11- Kuweka tawi la mti wa rangi ya kijani katika chumba ambapo maiti amekufa ndani yake.
12- Kusoma Qur-aan mbele ya maiti mpaka atakapoanza kuoshwa.
13- Kukata kucha za maiti na kunyoa nywele zake za chini.
14- Kuingiza pamba kwenye tupu ya nyuma ya maiti, mdomoni na kwenye pua.[3]
15- Kuweka mchanga kwenye macho ya maiti na kusema “Hakuna kinachoweza kujaza jicho la mwanaadamu isipokuwa mchanga.”
16- Watu wa maiti kuacha kula mpaka watakapomaliza kuzika.
17- Kudumu kulia mchana na usiku.
18- Mtu kukata nguo kwa kufiliwa na baba yake au ndugu yake.
19- Mtu kuhuzunika kwa maiti mwaka mzima. Mwanamke akawa (mwaka mzima wote ule) hajipaki hina, akawa havai nguo nzuri wala hajipambi. Mwaka ukamalizika, wakaanza sasa kujipamba na kufanya mambo ambayo yamekatazwa katika Shari´ah. Wanafanya hivyo wao na wale wanaoshirikiana nao kwa huzuni pamoja nao. Wanaita hilo “Kufunga huzuni.”
20- Baadhi ya watu wanaacha ndevu zao kwa ajili ya huzuni.
21- Kukunja mikeka na mabusati na vio vikafunikwa (ikawa hawajiangalii kwenye kio).
22- Kuacha kutumia maji yaliyo nyumbani ndani ya mitungi na vinginevyo. Kwa kuona kuwa ni najisi. Wanatoa ila ya kwamba roho ya maiti ikitoka huzama katika yale maji.
23- Anapopiga chafya mmoja wao katika chakula, wanasema “Zungumza na fulani au na fulani miongoni mwa wale walio hai katika wale anaowapenda.” Wanatia ila kwa hilo ili kule kupiga chafya kusije kumfika maiti.
24- Kuacha kula vitu vitamu na samaki kwa muda wa huzuni (msiba) wao kwa maiti wao.
25- Kuacha kula nyama, nyama za mishikaki na za kuchomwa.
26- Kauli ya Mutaswawwifah “Mwenye kumlilia yule aliyekufa, basi huyo atakuwa ametoka katika njia ya wale wajuzi!”
27- Kuacha nguo za maiti bila ya kuzifua mpaka siku ya tatu kwa madai ya kwamba kufanya hivyo kutamfanya asiadhibiwe na adhabu ya kaburi.
28- Baadhi yao wanasema “Atakayekufa siku ya Ijumaa au usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa, adhabu yake ya kaburi ni saa moja kisha anakatikiwa na adhabu na wala hairudi mpaka siku ya Qiyaamah.”
29- Kauli nyingine “Muumini ambaye ni muasi, adhabu inamkatikia siku ya Ijumaa na usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa. Haimrudilii mpaka siku ya Qiyaamah.”
30- Kutangaza kifo cha maiti juu ya mnara.
31- Baadhi ya watu pale ambapo wanapewa khabari ya kifo, husema “al-Faatihah kwa ajili ya roho ya fulani.”
Kuosha maiti
32- Kuweka kipande cha mkate na kopo la maji katika maeneo ambapo ameoshwa maiti kwa siku tatu baada ya kufa kwake.
33- Kuwasha taa au al-Qandiyl katika maeneo ambapo ameoshwa maiti kwa siku tatu, kuanzia pale ambapo jua linapochomoza mpaka pale linapozama. Watu wengine wanafanya hivyo kwa siku saba. Wengine wanazidisha siku hizi na wanafanya mfano wake – yaani kuwasha taa – katika maeneo ambapo maiti amekufa.
34- Muoshaji kusoma baadhi ya Dhikr miongoni mwa Adhkaar ambazo analeta katika kila kiungo anachokiosha (Adhkaar maalum).
35- Kusoma Dhikr kwa sauti ya juu wakati wa kuosha jeneza na pale linaposhindikizwa.
36- Kuziteremsha nywele za maiti (mwanamke) katikati ya matiti yake.
Sanda na kutoka na jeneza
37- Kumchukua maiti na kumpeleka sehemu ya mbali ili kwenda kumzika sehemu ya makaburi ya watu wema, kama (makaburi ya) Ahl-ul-Bayt na mfano wa watu kama wao.
38- Baadhi ya watu wanasema “Maiti hujifakhirisha kati yao ndani ya makaburi yao kwa zile sanda na uzuri wake. Wanatia ila ya sanda ya maiti ambayo si nzuri. Wanamtia aibu kwa hio.”
39- Kuandika jina la maiti – yaani kwenye sanda – na kwamba (maiti) huyo anashuhudia Shahaadah mbili na majina ya watu wa kwa nyumba ya Mtume (´alayhimus-Salaam) kwa mchanga wa Husayn (´alayhis-Salaam) ukipatikana na (mchanga huo) ukawekwa katika ile sanda.
40- Kuandika Du´aa katika sanda.
41- Kuipamba jeneza.
42- Kubeba bendera mbele ya jeneza.
43- Kuweka kilemba juu ya mbao. Kunaingia ndani ya hili kuweka kofia, mauwa ya harusi na kila kinachoonesha dalili ya ubora wa yule mtu.
44- Kubeba mauwa na picha ya maiti mbele ya jeneza.
45- Kuchinja mbuzi (au kondoo) wakati jeneza inapotolewa chini ya kuzingiti cha mlango. Baadhi ya watu wanaitakidi ya kwamba ikiwa watu hawakufanya hivyo kutakufa watu watatu katika hiyo nyumba.
46- Kubeba mkate na mbuzi mbele ya jeneza na kuichinja baada ya kuzika na kuigawa (nyama ya hiyo mbuzi) na mkate.
47- Baadhi ya watu wanaitakidi ya kwamba ile jeneza ikiwa ni ya mtu mwema huwa ni khafifu kwa wale wenye kuibeba na huenda haraka.
48- Kutoa Swadaqah pale ambapo jeneza inatolewa. Katika haya kunaingia kugawa vinywaji.
49- Kuanza kuibeba jeneza kwa mkono wa kulia.
50- Kuibeba jeneza hatua kumi katika kila upande katika pande nne (za jeneza).
51- Kuibeba (jeneza) polepole.
52- Msongamano katika jeneza.
53- Kuacha kutorudi katika jeneza.
54- Kuacha kuzungumza katika jeneza. Kunaingia ndani ya hili kunyanyua sauti kwa Dhikr – kama itakavyokuja baada yake – na kuzungumza watu wao kwa wao na mfano wa hayo.
55- Kusoma Dhikr kwa sauti, kusoma Qur-aan, Burdaa, Dalaail-ul-Khayraat na mfano wa hayo.
56- Kuleta Dhikr nyuma ya jeneza kwa kumtaja Allaah, Burdaa, Dalaail, al-Asmaa´ al-Husnaa.
57- Kusema nyuma ya jeneza “Allaahu Akbar Allaahu Akbar, ash-hadu an laa ilaaha illa Allaah yuhyi wa yumiyt, wa huwa hayyun laa yamuut. Subhanaa man ta´azaza bi qudrati wal baqaa´, wa qaharal ´ibaadah bil maut wal fanaa´.”
58- Kupiga kelele nyuma ya jeneza kwa kusema “Istaghfirlahu yaghfiruAllaahu lakum”.
59- Kupiga kelele kwa tamko la “al-Faatihah” wakati wa kupita katika kaburi la mtu mwema au njia za kupanda.
60- Mwenye kushuhudia jeneza anasema “Alhamdulillaahi ladhiy lam yaja´alniy minas-Sawaaid al-Mukhtaram” (Namshukuru Allaah Ambaye Hakunifanya katika wale ambao wamefikwa na mauti)
61- Baadhi ya watu wanaitakidi ya kwamba ile jeneza ikiwa ni ya mtu mwema inasimama (kivyake) kwenye kaburi la walii wakati inapita mbele yake pamoja na kuwa imebebwa.
62- Mtu kusema anapoliona lile jeneza “Hadhaa maa wa´adanaaAllaahu wa Rasuuluh, was-SwadaqahAllaahu wa Rasuuluh, Allaahumma zidnaa Iymaanan wa tasliymaa”.
63- Kufuata maiti kwa tetezo.
64- Kutufu kwenye ile jeneza pembezoni mwa makaburi.
65- Kutufu nayo (hiyo jeneza) kwenye Ka´abah mara saba.
66- Kutangaza jeneza kwenye milango ya Misikiti.
67- Kumuingiza maiti kwenye mlango wa “ar-Rahmah” katika Masjid-ul-Aqswaa na kuweka (ile maiti) kati ya mlango na as-Swakhrah. Wanakusanyika baadhi ya Mashaykh wakisoma baadhi ya Adhkaar.
68- ar-Rathaa (kutaja sifa za maiti baada ya kufa) wakati jeneza inapoletwa Msikitini kabla ya kumswalia au baada yake. Au kabla ya kuchukua ile jeneza au baada ya kuzika ile maiti.
69- Kujilazimisha (kudumu kwa) kubeba jeneza kwenye gari na kuishindikiza kwenye gari.
70- Kubeba baadhi ya maiti kwenye kifaru.
Kumswalia
71- Kuswalia Swalat-ul-Ghayb jeneza za Waislamu ambao wamekufa mbali kila siku baada ya jua kuchomoza.
72- Kumswalia maiti aliyekufa mbali pamoja na kujua ya kwamba amekwishaswaliwa katika maeneo alipo.
73- Baadhi yao wanasema wakati wanapomswalia “Subhaana man qahra ´ibaadata bil maut, Subhaana Al-Hayy alladhiy laa yamuut”.
74- Kuvua viatu wakati wa kumswalia hata kama (viatu hivyo) vitakuwa havina najisi kisha akasimama juu ya vile viatu.
75- Imamu kusimama katikati ya mwanaume (ikiwa maiti ni mwanaume) na kwenye kifua cha mwanamke (ikiwa maiti ni mwanamke).
76- Kusoma Du´aa al-Istiftaah.[4]
77- Kuacha (au kuchukia) kusoma Suurat-ul-Faatihah na Suurah nyingine.
78- Kuacha kutoa Salaam.
79- Baadhi ya watu baada ya kumswalia wanasema kwa sauti ya juu “Mnamshuhudia nini (maiti)?” Walioko pale waseme “Alikuwa ni katika watu wema na mfano wa hayo”.
Kuzika na yanayofungamana na kuzika
80- Kuchinja nyati wakati jeneza inapofika kwenye makaburi kabla ya kuzikwa na kugawa ile nyama kwa wale waliohudhuria.
81- Kuweka damu ya kile kilichochinjwa wakati jeneza inapotoka katika nyumba kwenye kaburi la maiti.
82- Kuleta Dhikr pembezoni mwa maiti kabla ya kuzika.
83- Kuadhini wakati maiti anapoingizwa katika kaburi.
84- Kumteremsha maiti katika kaburi kwa upande wa kichwa cha kaburi.
85- Kuweka kitu katika mchanga wa Husayn (´alayhis-Salaam) pamoja na maiti wakati wa kuteremshwa kwenye kaburi, kwa kuwa (ule mchanga) ni amani ya kila khofu.
86- Kuweka mchanga chini ya maiti bila ya dharurah.
87- Kuweka mto au mfano wa mto chini ya kichwa cha maiti kwenye kaburi.
88- Kuingiza (kurusha) maji ya waridi kwa maiti kwenye kaburi lake.
89- Walioko pale kurusha mchanga hali ya kusema “Inna lillaahi wa inna ilayhi raaji´uun”.
90- Kusoma “Minhaa khalaqnaakum” wakati anaporusha fungu la kwanza, “Wa fiyhaa nu´iydukum” anapoteka mara ya pili, “Wa minhaa nukhrijukum taaratan ukhraa” anapoteka mara ya tatu.
91- Kusema katika kofi la kwanza “Bismillaah”, la pili “al-Mulk lillaah”, la tatu “al-Qudrat lillaah”, la nne “al-´Izzah lillah”, la tano “al-´Afuu al-Ghufraanu lillaah”, la sita “ar-Rahmatu lillaah” kisha mara ya saba anasema “Kullu man ´alayhaa faan... “ na anasoma Kauli Yake (Ta´ala): “Minhaa khalaqnaakum... “.
92- Kusoma Suurah saba “al-Faatihah, al-Mu´awwidhatayn,[5] al-Ikhlaasw, Ithaa jaa-a nasrullaahi, Qul yaa ayyuhal-Kaafiruun na inna anzalna na Du´aa hii “Allaahumma inni as-aluka bismika al-´Adhwiym, wa as-aluka bismika ladhiy huwa qiwaamud-Diyn, wa as-aluka... , wa as-aluka... , wa as-aluka... , wa as-aluka bismika ladhiy ithaa su-ilta bihi a´atwayta, wa ithaa du´iyta bihi ajabta, Rabba Jibriyl wa Israafiyl wa ´Izraail... Yote haya wakati anapozikwa maiti.
93- Kusoma Suurat-ul-Faatihah kwenye kichwa cha maiti na mwanzo wa Suurat-ul-Baqarah kwenye miguu yake.
94- Kusoma Qur-aan wakati maiti anapofunikwa na mchanga.
95- Kumlakinia maiti.
96- Kuweka mawe mawili kwenye kaburi la mwanamke.
97- ar-Rathaa (kumsifu maiti) baada ya kuzikwa maiti kwenye kaburi.
98- Kumchukua yule maiti kabla ya kumzika au baada yake kumpeleka katika makaburi ya watu watukufu.
99- Kukaa kwa maiti baada ya kumzika katika nyumba ya udongo (mchanga).
100- Kuzuiawa wale ambao wameenda kuzika kuingia kwenye nyumba wanaporejea kutoka kuzika mpaka waoshe viungo vyao kutokana na athari ya maiti.
101- Kuweka chakula na maji juu ya kaburi ili watu wayachukue.
102- Kutoa Swadaqah kwenye kaburi.
103- Kunyunyiza maji juu ya kaburi lake upande wa kichwa chake, kisha yakanyunyiziwa pembezoni na mtu mbora akanyunyizia katikati yake (maiti).
Taazia (kutoa pole) na yanayofungamana na taazia
104- Kutoa pole kwenye makaburi.
105- Watu kukusanyika mahala pa kutoa pole (matanga).
106- Kuiwekea mpaka taazia kwa siku tatu.
107- Kuacha kulala kwenye magodoro ambayo yanawekwa katika nyumba ya maiti ili wapate kukaa wale waliokuja kwa ajili ya kutoa pole au yakaachwa namna hiyo mpaka kupite siku saba, baada ya hapo wayaondoe (warudi katika hali ya kawaida, kuyalalia).
108- Kutoa pole kwa kusema “A´adhwama Allaahu la ajra, walhamaka bis-Swabra, wa razaqanaa wa iyyaaka as-Shukraa... “ mpaka mwisho wa Du´aa hii.
109- Kutoa pole kwa kusema “Inna fiyllaahi ´azaa-a, min kulli muswiybatin, wa khalafan min kulli faaitin, fabillaahi fathiquu, wa iyyahu farjuu, fa inna maa mahruum man huruumu man hurima thawaaba”.
110- Watu wa maiti kuwapikia wageni chakula.
111- Wageni kuja kwa ajili ya maiti siku ile ya kwanza, ya saba na ya arubaini.
112- Watu wa maiti kupika chakula ile Alkhamisi ya kwanza.
113- Kuitikia wito (mualiko) wa chakula wa watu wa maiti.
114- Baadhi ya watu kusema “Asiondoe meza ya chakula zile siku tatu isipokuwa yule aliyeiweka”.
115- Kufanya au kununua vitu tamtam na vitavyokuliwa na hiyo tamtam katika siku ya saba.
116- Mtu kuacha anausia watu wapike chakula na wageni siku ya kufa kwake au baada yake na kutoa pesa nyingi kwa yule atakayesoma Qur-aan kwa ajili yake yeye au akafanyiwa Tasbiyh au Tahliyl.
117- Mtu kuacha anausia akifa walale kwenye kaburi lake watu kwa siku arubaini, zaidi ya hapo au chini ya hapo.
118- Mtu kutoa Waqf na khaswa ili asomewe Qur-aan Tukufu au aswaliwe Swalah za Nawaafil (Sunnah), au afanyiwe Tahliyl, au mtu amswalie Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kunuia thawabu zimwendee aliyetoa Waqf ule au yule aliyemtembelea.
119- Walii wa maiti kumtolea Swadaqah kabla ya kupita siku kwa kitu kitachomkulia na wepesi. Lau hatopata (au hawezi) basi amswalie Rakaa mbili na amsomee katika kila Rakaa al-Faatihah na Aayat-ul-Kursiy mara moja, Suurat-ut-Takaathur mara kumi. Akimaliza aseme “Allaahumma swallaytu haadhihi Swalaah wa ta´alam maa aradwtu bihaa, Allaahumma ba´ath thawaabahaa ilaa qabri fulaan al-mayyit” (Ee Allaah! Hakika mimi nimeswali Swalah hii na Wewe unajua ninachokusudia kwa Swalah hii. Ee Allaah! Tuma thawabu zake kwenye kaburi la fulani na fulani ambaye ni maiti)
120- Kumtolea Swadaqah maiti kutokana na kile chakula alichokuwa anapenda maiti.
121- Kumtolea Swadaqah maiti kwa miezi mitatu: Raajab, Sha´baan na Ramadhaan.
122- Kukatika (kubomoka) kwa Swalah.
123- Kuwasomea maiti (Qur-aan).
124- Kumfanyia maiti Tasbiyh.
125- Kumuacha mtumwa huru.
126- Kumsomea maiti Qur-aan na kukhitimisha kwenye kaburi lake.
127- Kufanya as-Swubhah kwa ajili ya maiti. Nako ni kule kuamka kwao mapema kwenda kwenye kaburi la maiti wao ambaye walimzika jana, jamaa zao na marafiki zao.
128- Kutandika busati na vinginevyo kwenye udongo (au mchanga) kwa wale watakaokuja katika as-Swubhah.
129- Kuweka hema juu ya kaburi.
130- Kulala kwenye kaburi siku arubaini, chini ya hapo au zaidi ya hapo.
131- Kutaja khabari za kuhusu maiti usiku wa arubaini au kila mwaka siku ile aliyokufa, inayoitwa “at-Tadhkaar”.
132- Kuchimba kaburi kabla ya kufa na kujiandaa nalo.
Kuyetembelea makaburi
133- Kwenda kutembelea makaburi baada ya kufa kwa siku tatu na wanaita “al-Farqa” na kwenda kutembelea makaburi mwanzoni wa kila wiki, kisha siku ya kumi na tano, kisha siku ya arubaini na wanaita hilo “at-Twala´aat”. Na miongoni mwao kuko ambao wanafupisha zile siku za mwisho mbili.
134- Kwenda kutembelea makaburi ya wazazi wawili kila siku ya Ijumaa.
Hadiyth iliyopokelewa juu ya masuala haya ni maudhuu´.
135- Baadhi yao wanasema “Yule maiti endapo watu hawakutoka kwenda kumtembelea usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa hubaki akiwa ni maiti mnyonge mbele ya maiti wenzake na wanadai kuwa yule maiti anawaona pale wanapotoka”.
136- Wanawake kwenda wakikusudia (Msikiti wa) Jaamiy´ al-Amawiy wakati wa giza katika usiku wa Jumamosi mpaka siku ya pili mchana wakati wa Dhuhaa ili kutembelea makaburi ya al-Yahyawiy na wanadai ya kwamba kwenda kule kukariri kitendo kama hichi Jumamosi arubaini mtu analipwa kulingana na nia aliyoweka.
137- Kukusudia kaburi la Ibn ´Arabiy Suufiy kwa Ijumaa arubaini kwa madai ya kwamba mtu akifanya hivyo atatatuliwa haja.
138- Kutembelea makaburi siku ya ´Aashuuraa.
139- Kutembelea makaburi siku usiku wa kuamkia Nifsu Sha´baan na kuwasha moto kwenye kaburi.
140- Kwenda kwao kwenye makaburi siku ya Idi, Raajab, Sha´baan na Ramadhaan.
141- Kwenda kwao kutembelea makaburi siku ya Idi.
142- Kwenda kwao kutembelea makaburi siku ya Jumatatu na Alkhamisi.
143- Kusimama kwa baadhi ya wale wenye kutembelea makaburi kidogo kwa unyenyekevu mkubwa kwenye mlango (wa makaburi) kana kwamba wanaomba idhini, kisha ndio wanaingia.
144- Kusimama mbele ya kaburi akiweka mikono yake kama mwenye kuswali kisha ndio anakaa.
145- Kutayamamu kwa ajili ya kutembelea makaburi.
146- Kuswali Rakaa mbili wakati wa kwenda kutembelea. Anasoma katika kila Rakaa al-Faatihah na Aayat-ul-Kursiy mara moja na Suurat-ul-Ikhlaasw mara tatu na anafanya thawabu kumuendea maiti.
147- Kusoma Suurat-ul-Faatihah kwa ajili ya maiti.
148- Kusoma Suurat Yaasin kwenye makaburi.
149- Kusoma “Qul huwaAllaahu Ahad” mara kumi na moja.
150- Du´aa kwa kusema kwake “Allaahumma inni as-aluka bihurumat Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) an laa tu´addhib haadhal-mait”.
151- Kulitolea Salaam (kaburi) kwa tamko “´alaykumus-Salaam” au “as-Salaam ´alaykum”.
152- Kwenda kusoma kwenye makaburi ya manaswara na mayahudi “Za´amaa ladhina kafaruu anllan yuba´athuu... ”.
153- Kutoa mawaidha juu ya minbari na kwenye viti kwenye makaburi katika siku za mwezi (tarehe 13, 14 na 15).
154- Kupiga kelele kwa Tahliyl kwenye makaburi.
155- Kuwaita wale wenye kutembelea makaburi kuwa ni “Hajj”.
156- Kuwatumia Salaam Mitume (´alayhimus-Salaam) kwa wale wenye kuwatembelea.
157- Wanawake wanaenda siku ya Ijumaa kutembelea makaburi as-Swaalihiyyah (Damasqus, Syria) na wakashirikiana kwa hilo na wanaume kwa tabaka mbalimbali.
158- Kutembelea athari za Mitume zilizoko Shaam. Kwa mfano athari za Ibraahiym (´alayhis-Salaam) na athari tatu zilizoko katika jabali Qasbuun Gharbiy ar-Ribwah.
159- Kwenda kutembelea kaburi la askari asiyejulikana au shahidi asiyejulikana.
160- Kutoa zawadi thawabu za ´Ibaadah, kama Swalah na kusoma Qur-aan kwa maiti za Waislamu.
161- Kutoa zawadi za ´amali kumpa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
162- Kumpa malipo yule mwenye kusoma Qur-aan na kumpa zawadi (thawabu hizo) maiti.
163- Kusema mwenye kusema “Hakika Du´aa ni yenye kukubaliwa kwenye makaburi ya Mitume na watu wema”.
164- Kulikusudia kaburi ili kwenda kusoma Du´aa mbele ya kaburi hilo kwa kutaraji kujibiwa (Du´aa hiyo).
165- Kuyafunika makaburi ya Mitume, watu wema na wengineo.
166- Baadhi ya watu wanaitakidi kuwa kaburi la mtu mwema linapokuwa katika kijiji kwa baraka za kaburi lile wanaruzukiwa (watu wa kijiji hicho) na kunusuriwa. Na wanasema “Yeye ndio nguzo (neema) ya mji” kama wanavyosema “Sayyidah Nafiysah ni nguzo katika Qaahirah na “Shaykh Raslaan ndio nguzo Dimashq” na “fulaani na fulaani ndio nguzo ya Baghdaad” na wengineo”.”
167- Kuitakidi kwao katika makaburi mengi ya mawalii kwamba wana mambo maalum kama mambo maalum yanayopatikana kwa matabibu. Miongoni mwao kuko wanaonufaisha kwa maradhi ya macho na wengine wananufaisha kwa maradhi ya homa...
168- Baadhi yao wanasema “Kaburi ambayo inajulikana kupona maradhi ya “at-Tiryaaq”.
169- Baadhi ya Mashaykh kusema kwa wale viongozi “Ikiwa wewe una haja kwa Allaah, basi taka msaada kutoka kwangu” au wanasema “Taka msaada kutoka kwenye kaburi langu”.
170- Kutukuza vitu vilivyo pembezoni mwa kaburi la walii, katika miti na mawe na kuitakidi ya kuwa yule atakayekata kitu chochote atafikwa na madhara.
171- Baadhi yao wanasema “Mwenye kusoma Aayat-ul-Kursiy na akaelekea upande (alipozikwa) ´Abdul-Qaadir al-Laylaaniy na akamtolea Salaam mara saba, basi kwa kila Salaam moja aliotoa ataondolewa haja zake”.
172- Kunyunyizia maji kwenye kaburi la mke ambaye amefiwa na mume wake ambaye (mume) alimuoa baada yake, kwa kudai ya kwamba akifanya hivyo atapunguza ule moto wa ule wivu.
173- Kusafiri kwenda kutembelea makaburi ya Mitume na watu wema.
174- Kupiga ngoma (matari), tarumbeta, firimbi na kucheza kwenye kaburi la Ibraahiym (´alayhis-Salaam) kwa kujikurubisha kwa Allaah.
175- Kutembelea kaburi la Ibraahiym (´alayhis-Salaam) ndani ya jengo.
176- Kujenga majumba kwenye makaburi na kueshi ndani yake.
177- Kujenga (majengo ya) mawe au mbao kwenye makaburi.
178- Kuweka ad-Daraabiziyn kwenye makaburi.
179- Kulipamba kaburi.
180- Kubeba msahafu kwenye makaburi na kumsomea maiti kutoka kwenye msahafu huo.
181- Kuweka misahafu kwenye makaburi kwa yule mwenye kukusudia kwenda kusoma Qur-aan kule.
182- Kupamba zile kuta za makaburi na zile nguo zake.
183- Kutanguliza mashtaka (matatizo, dhiki n.k.) kwa kuyaandika kwenye karatasi na kuyaweka ndani yake, kwa kudai kuwa mwenye kaburi hilo atayatatua.
184- Kufunga vitambaa kwenye madirisha ya makaburi ya mawalii ili kuwakumbusha na kutatuliwa haja zao.
185- Wale wenye kutembelea mawalii kugonga ngoma zao na kuzitundika.
186- Kuweka mataa na nguo juu ya kaburi kwa makusudio ya kutaka baraka.
187- Baadhi ya wanawake kujisugua kwenye kaburi na kujisugua sehemu ya siri ili aweze kupata mimba kwenye kaburi.
188- Kuligusa kaburi na kulibusu.
189- Mtu kuambatanisha tumbo lake na mgongo na ukuta wa kaburi.
190- Mtu kuambatanisha mwili wake au kitu katika mwili wake na kaburi au kilichoko karibu na kaburi katika udi na mfano wake.
192- Kutufu makaburi ya Manabii na watu wema.
193- Mtu kujitambulisha kwenye kaburi. Nako ni kukusudia kaburi la baadhi ya wanaozingatiwa wana dhana nzuri siku ya ´Arafah na mkusanyiko mkubwa mbele ya kaburi lake kama ilivo katika ´Arafah.
194- Kuchinja na kufanya Udhhiyah kwenye kaburi.
195- Kuelekea upande ambapo yupo (amezikwa) mtu mwema wakati wa kuomba Du´aa.
196- Kujizuia kuipa mgongo upande ambapo kuna baadhi ya watu wema (waliozikwa).
197- Kuyakusudia makaburi ya Mitume na watu wema kwa kuwaomba Du´aa huku mtu akitaraji kujibiwa.
198- Kukusudia kwenda kuswali kwenye kaburi.
199- Kukusudia kwenda kuswali kwa kuelekea kaburi.
200- Kukusudia kwenda kufanya Dhikr, kusoma, kufunga na kuchinja (kwenye makaburi).
201- Kutawassul kwa Allaah (Ta´ala) kupitia kwa waliozikwa kwenye makaburi.
202- Kuapa kwa aliyekufa kwa Allaah.
203- Kuambiwa yule maiti au mtu asiyekuwepo katika Mitume na watu wema “Muombe Allaah”.
204- Kutaka msaada kutoka kwa maiti. Kama kusema kwao “Ee Bwana wangu fulani! Niokoe au ninusuru kutokana na adui yangu.”
205- Kuitakidi ya kwamba yule maiti anayaendesha mambo asiyekuwa Allaah.
206- Kukaa I´itikaaf mbele ya kaburi na kujikurubisha nalo.
207- Kutoka kwenda kutembelea makaburi ambayo wanayaadhimisha kwa nyuma.
208- Baadhi ya al-Mudarwishiyn[6] husema wanaotoka katika miji na kwenda hususan kutembelea makaburi ya mawalii na maiti wakati wa kurejea kwenye miji yao “al-Faatihah kwa ajili ya wakazi wote wa mji huu kwa Sayyid (Bwana) fulani” na wanawataja wale mabwana, kuwategemea, akiwaashiria na akifuta uso wake.
209- Kusema kwao “as-Salaam ´alayka yaa waliyyuAllaah, al-Faatihah, ziyaadat-us-Sharaf an-Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wal arbaa´, wal aqtwaar, wal anjaab, wal autaad, wa hamalat al-Kitaab wal aghwaathi... “
210- Kulienua kaburi na kulijengea.
211- Mtu kuacha anausia ajengewe juu ya kaburi lake.
212- Kuweka chokaa kaburi.
213- Kuliandika kwa marembo jina la maiti na tarehe ya kufa kwake juu ya kaburi.
214- Kujenga Misikiti na minara juu ya makaburi.
215- Kuyafanya makaburi ni Misikiti kwa kupaswalia na ndani yake.
216- Kumzika maiti Msikitini au kujenga Msikiti juu yake (kaburi lake).
217- Kuelekea kaburi wakati wa Swalah na kuipa mgongo Ka´abah.
218- Kuyafanyia makaburi sherehe.
219- Kuweka al-Qindiyl juu ya kaburi ili watu waweze kuyajia na kuyatembelea.
220- Kuweka mafuta na mshumaa kwa ajili ya kuliwashia taa kaburi, au jabali au mti.
221- Kukusudia watu wa Madiynah kulitembelea kaburi la Mtume kila wanapoingia Msikitini au wanapotoka.
222- Kusafiri kwa ajili ya kulitembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
223- Kumtembelea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mwezi wa Raajab.
224- Kuelekea upande wa kaburi lake wakati wa kuingia kwenye Msikiti (wa Mtume) na kusimama mbali na kaburi kwa kuwa na unyenyekevu na kuweka mkono wake wa kulia juu ya wa kushoto kana kwamba yuko katika Swalah.
225- Kumuomba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mswamaha na kusoma Aayah “Wa lau annahum idhdhwalamuu anfusahum jaa-uka fastaghfaruAllaahu... ”
226- Kutawassul kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
227- Kuapa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
228- Kutaka msaada badala ya Allaah (Ta´ala).
229- Kukata nywele zao na kuziweka katika al-Qindiyl kubwa ilioko karibu na kaburi ya udongo (mchanga) wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
230- Kuligusa (au kulipapasa) kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
231- Kulibusu.
232- Kulitufu.
233- Kuambatanisha tumbo au mgongo kwa kuta za kaburi lake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
234- Kuweka mkono kwenye dirisha la chumba cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mtu akaapa “Wa haqqa ladhiy wadhwa´ata yadaka ´alaa shubbakihi” (Kwa haki ya yule ambaye aliyeweka mkono wake kwenye dirisha lake) na mtu aseme “ash-Shafaa´ah yaa RasuulaAllaah” (Ewe Mtume wa Allaah! Naomba uombezi)
235- Kurefusha kisimamo kwenye kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ajili ya kujiombea Du´aa huku ameelekea chumba chake.
236- Kujikurubisha kwa Allaah kwa kula tende as-Swayhaaniy katika ar-Rawdhwah baina ya kaburi na minbari.
237- Kukusanyika kwenye kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ajili ya kusoma Khitmah na kuimba Qaswiydah.
238- Kuomba kunyweshelezwa kwa kulifunua kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au mwingineo katika makaburi ya Mitume na watu wema.
239- Kutuma (au kupeleka) makaratasi ndani yake mtu anamuomba haja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
240- Baadhi yao wanasema “Hakika inatakikana mtu asitaje haja zake na kuomba mswamaha wa madhambi yake kwa mdomo wake wakati wa kutembelea kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anajua zaidi haja na manufaa yake kuliko yeye”.
241- Kusema kwake “Hakuna tofauti baina ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwa kwake hai katika kushuhudia (kuona) Ummah wake, kujua hali zao, nia zao na yale yanayowasibu”.
Haya ndio ya mwisho niliyokuwa na wepesi wa kuyakusanya katika Bid´ah za jeneza.
Alhamdulillaahi. Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, ahli zake na Maswahabah zake wote.
[1] Neno kumlanikia bi maana ni kule kumwambia anayetaka kukata roho kutamka shahaadah
[2] Yaani maimamu wa Shiy´ah ambao wao wanaamini kuwa wamekingwa na madhambi.
[3] Isipokuwa katika hali zinazotokea. Kama kwa mfano maiti awe na ila fulani inayokhofiwa kutokwa na kitu kinachoweza kuichafua ile sanda au kuiweka najisi.
[4] Du´aa ya kufungulia Swalah
[5] al-Ikhlaasw na al-Falaq
[6] Kundi katika Masufi